" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Wednesday, October 15, 2008

 Tumejifunza nini kutokana na uchaguzi mdogo Tarime?

KAMPENI rasmi za uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime zilianza Septemba 21. Kampeni hizo zilizofanyika kwa wiki tatu mfululizo hadi kukoma siku moja tu kabla ya uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita, Oktoba 12 kwa hakika ziliwasimamisha dede Watanzania.

Kila kukicha habari za kutoka Tarime zilipamba vichwa vya habari vya magazeti, nyingi hazikuwa za kufurahisha, zaidi ni vitisho na wasiwasi kwamba Tarime hapatoshi!

Vijembe na kejeli mara hii havikufua dafu kwani vilizidiwa na mapanga na mawe. Wengi walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha yao. Kama vile haitoshi hata kiumbe asiyejua kitu kuhusu uchaguzi, mbwa aliyevishwa sare ya CCM, alikatishwa maisha yake kutokana na ushabiki usio wa kistaarabu. Tuliouona Tarime haukuwa ushabiki wa kisiasa bali wa kihuni. Tulisahau kauli mbiu ya kushindana bila kupigana.

Katika hali ya kawaida hiyo haikuwa demokrasia na pengine ni vigumu kuuita uchaguzi ule kuwa ulikuwa huru, pengine ulikuwa wa haki lakini haukuwa wa amani. Yaliyotokea Tarime yanaakisi hali ya kutokuwapo kwa demokrasia halisi Tanzania. Demokrasia yetu bado ni ya ‘magubegube’ (ya kubabaisha). Bado tunadhani kwamba ushindi ni lazima, wanasiasa wanajaribu kila mbinu kuhakikisha ushindi bila ya kuheshimu utashi wa wananchi. Bado wako wanaodhani kwamba wana haki ya kutawala au kuchukua viti vyote vya uwakilishi. Bado demokrasia haijatuingia akilini mwetu kwamba ni uhuru wa kuchagua kiongozi unayemtaka.

Bado tunadhani tunaweza kushinda kwa njia za wizi na ulaghai. Bado tunafikiria kuwa kinachotakiwa ni ‘ushindi wa kishindo’ kumbe vile wananchi wanachotaka ni mwakilishi wao atakayetetea maslahi yao.

Napenda kuungana na wale wenye maoni ya kwamba demokrasia ya vyama vingi kwa Afrika ni demokrasia ngeni, pengine tunahitaji muda zaidi wa kujifunza au pengine si demokrasia stahiki kwa watu wa Bara hili wenye miundo yao ya asili ya utawala.

Inaonyesha kana kwamba demokrasia hii tuliyonayo ni demokrasia ya kupandikizwa na kulazimishwa kwetu, wenyewe hatujawa tayari. Hata hivyo, bado hatujachelewa, kama kweli tunaipenda na tunataka iingie katika mizizi ya mifumo yetu ya uongozi wa umma, basi tuwe tayari kujifunza na katika kujifunza tujitahidi kujiepusha na mabaya, kwa mfano kutumia nguvu wakati wa kampeni na wakati wa uchaguzi, kutumia nguvu za dola za ziada na hata kufanya mbinu za kupata ushindi usio halali. Hayo ni mambo ambayo kama kweli tunayo dhamira ya kufuata mfumo huu wa demokrasia uliopandikizwa kwetu, mambo hayo yamo ndani ya uwezo wetu.

Demokrasia hii tunayoiga haitaki mizengwe, ina misingi yake iliyo bayana, demokrasia hii haihitaji risasi wala mabomu. Lakini ni demokrasia inayopaswa kufuatwa na watu wote katika jamii, wapiga kura, wanasiasa na hata Serikali. Kama tutaizingatia misingi hiyo ya demokrasia ni wazi kwamba tutajiepusha kwa kiasi kikubwa na tafrani zinazotokea wakati wa uchaguzi.

Binafsi nadhani hatuhitaji Jumuiya ya Ulaya ituambie la kufanya, hatuhitaji wakaguzi wa nje waje watwambie kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki. Hatuhitaji kufundishwa hayo, kwani hayo yamo ndani ya uwezo wetu, ni utashi na matakwa yetu na ni ustaarabu tunaoweza kuujenga tukitaka.

Lakini kuna jingine, ambalo pengine ni funzo kwa Chama tawala, kwamba wananchi wanaposema ‘hapana’ maana yake ni ‘hapana.’ Tarime wametupa fundisho, wananchi wa Tarime pengine ukali ni khulka yao, ni watu wasiokubali kunyanyaswa wala kuonewa, ni watu walio tayari kusimamia haki zao hata kama ikibidi wengine kupoteza maisha yao, hiyo ndiyo gharama ya demokrasia, lakini gharama hii ni kubwa mno na ambayo tunapaswa kuhakikisha kwamba hatuingii katika gharama za aina hiyo katika chaguzi zozote zile ziwazo hapa nchini.

Lakini twapaswa kufahamu kwamba Watanzania kuna kitu wamejifunza kutoka Tarime na kama wataamua kutumia mbinu kama za wakazi wa Tarime katika kuhakikisha kwamba wanalinda haki yao ya kuchagua, basi bila shaka Tanzania patakuwa hapakaliki, patachimbika bila jembe!

Watawala na viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa waheshimu matakwa ya wananchi na wawape uhuru wao wa kuchagua. Hakuna ubishi kwamba kila anayeingia katika ushindani anaingia kwa dhamira ya kushinda, lakini kushinda huko hakupaswa kuwe ‘kwa kucha na meno!’ Mwageni sera zenu wananchi watazisikia. Kwanini hatuchukui mfano wa biashara? Wafanyabiashara kama 10 wanakuwa wamejipanga katika mstari mmoja na pengine wote wanauza bidhaa za aina moja, lakini wakati huo huo wanaheshimu utashi wa wateja wao. Mteja anaweza kumruka mfanyabiashara wa kwanza na akaenda kwa mfanyabiashara wa katikati au wa mwisho. Na hiyo ndiyo dhana ya biashara huria na pia inapaswa iwe dhana ya siasa huria.

Lakini pia kama ambavyo kwenye biashara zipo za ‘kimachinga’ ambazo mmachinga utakapomuuliza bei ya kitu ni lazima ukinunue, usipokinunua utavurumishiwa gunia la matusi mpaka utamani ardhi ipasuke ujifukie. Na siasa nazo ziko za namna hiyo pia, zile za Tarime ukiwa ni mfano mmoja wapo.

Tunakumbuka jinsi Mwenyekiti wa DP, mchungaji Christopher Mtikila alivyovurumishiwa mawe, kisa eti alitamka yasiyowaridhi wana-Tarime. Hizo ni siasa za ‘kimachinga’ lazima ukubaliane na wanayoyataka wachuuzi. Lakini hiyo ni ilani iliyo kiambazani inapaswa kuzingatiwa, tayari moshi umeshaanza kufuka, tutahadhari nyika zisishike moto!

0754 849694
hshamte@mwananchi.co.tz

1 Maoni ya Wasomaji:

Blogger Mzee wa Changamoto anasema...

Labda tumejifunza kuwa safari ijay, tuwe na pesa za kutosha, tutangulize makada wa kutosha na pia tuhonge kulingana na mazingira.
Kwani suala si kutetea wananchi, bali ni kutawala.
Blessings

2:34 AM  

Post a Comment

<< Rudi mwanzo

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

  • The Citizen
  • Mwananchi
  • Mwanaspoti
  • Business Times
  • Majira
  • Daily News
  • Nipashe
  • The Guardian
  • The Express
  • Kiongozi
  • Uhuru/Mzalendo
  • Arusha Times
  • BLOGI ZA KISWAHILI

  • Bangaiza
  • Mwandani
  • Pambazuko
  • Damija
  • Mtafiti
  • Martha
  • Gaphiz
  • Swahili time
  • Miruko
  • Dira yangu
  • Msangimdogo
  • Jeff Msangi
  • Kasri la mwanazuoni
  • Kurunzi
  • Baragumu
  • Mawazohuru
  • Fikra Thabiti
  • Mtandaoni
  • Motowaka
  • Mkwinda
  • Ngurumo
  • Nyembo
  • Bwaya
  • Omega
  • Tafakari za Maisha
  • Nuru akilini
  • Mtandawazi
  • Mhujumu
  • Vijimamboz
  • Wakati wa Ukombozi
  • Kijiwe Joto
  • Watoto Wetu
  • Jungu kuu
  • Kisima cha Weledi
  • Jarida la Ughaibuni
  • Bhalezee
  • Sauti ya Baragumu
  • Kona yangu
  • Furahia Maisha
  • Bakanja
  • Terrie Swai
  • Fatma Karama
  • Kazonta
  • Binti Afrika
  • Blogu ya Kilimo
  • Ukombozi
  • Mwafrika
  • Digital Africa
  • Blogu ya lugha mseto
  • BLOGI ZA WAAFRIKA

  • BLOGAFRICA
  • BLOGU ZA WAAFRIKA
  • DIGITAL AFRICA
  • MAMA JUNKYARD'S
  • MSHAIRI
  • KENYAN PUNDIT
  • MONGI DREAMS
  • ISARIA MWENDE
  • CUNNING LINGUISTICA
  • ETHIOPUNDIT
  • MOCHALICIOUS
  • UNGANISHA
  • DEMOKRASIA KENYA
  • CHANUKA
  • BANKELE
  • MAARIFA/AKIEY
  • AFROMUSING
  • NEHANDA DREAMS
  • BLACK LOOKS
  • YUMMY WAKAME
  • AFRICAN OIL POLITICS
  • NUBIAN SOUL
  • SANAA
  • VIRTUAL INSANITY
  • MENTAL ACROBATICS
  • KENYA UNLIMITED
  • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

    April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

    Imetengenezwa na

    Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

    na inawezeshwa na