" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Thursday, July 31, 2008

 Mfumo wa uongozi na demokrasia Afrika, ni mkorogovyogo!

Na Hawra Shamte

UKIANGALIA mlolongo wa matukio, visa na mikasa ya viongozi wa Bara la Afrika, moja kwa moja utabaini kuwa mengi wafanyayo ni yale yaliyoainishwa katika falsafa za Niccolo Machiaveli, mwanafalsafa wa karne ya 15 aliyezaliwa Roma Italia.
Katika masuala ya uongozi wa umma, Machiaveli aliweka mkazo kwa kiongozi kung’ang’ania kuendelea kubaki madarakani, alisisitiza kwamba ‘ufalme’ au uongozi ni lazima ulindwe kwa nguvu zote, hata ikibidi kutumia jeshi ama kuua.
Kama ni utashi wao, viongozi wengi hasa wa Bara la Afrika wangependa waendelee kukaa madarakani daima dawama, kwao wao ukishakamata madaraka ni sawa na pingu za maisha, hadi ufe uzikwe.
Mifano tunayo mingi, Wapo akina Yoweri Museveni, Robert Mugabe, Omar Al Bashir, Husni Mubarak na wengineo. Sidhani kwamba ni lazima wajitangaze kuwa ni maraisi wa maisha, bali vitendo vyao vinatosha kuthibitisha hayo. Je, demokrasia ya uchaguzi na kupishana madarakani inatumikaje Afrika?
Pengine demokrasia ya aina hiyo si demokrasia ya waafrika, uongozi wa jadi ungetosha kujenga misingi ya uongozi na demokrasia, kwani hivyo ndivyo inavyoonyesha kihalisia. Kila anayeshika madaraka ikiwa atalazimika kuondoka madarakani ataweka mazingira ambayo kama ataondoka basi nafasi yake ishikwe na angalau na mtoto wake, mifano ya hao tunayo mengi.
Tumeshuhudia katika nchi nyingi za Kiafrika viongozi wakiwa wanabadilisha katiba, za nchi ilimradi tu waendelee kubaki madarakani, hata kama wananchi wameshawachoka. Mara ngapi tunasikia kwamba Rais fulani anataka kufanya mabadiliko ya katiba ili kuongeza muda wa Rais kukaa madarakani.
Ziko katiba zinazoweka vipindi vya urais, kwa mfano Tanzania kipindi cha Rais kukaa madarakani ni miaka mitano mara mbili, hii ina maana ya kwamba baada ya miaka kumi hata kama rais huyo anapendwa vipi ni lazima akabidhi uongozi kwa mwingine.
Uamuzi wa aina hiyo una faida zake na hasara zake, faida ni kwamba unaepusha kujenga himaya ya kifalme na kidikteta. Hasara yake ni kwamba mara nyingine inashindikana kumaliza ajenda na miradi ambayo Rais amejiwekea kwani miaka 10 si mingi na sera nyingi ni za muda mrefu.
Yawezekana mtu akajenga hoja kwamba uongozi ni mchakato, hivyo wengine watakaokuja badala ya aliyeondoka watauendeleza mchakato huo. Hiyo ni kweli na ndivyo inavyopaswa iwe, lakini si lazima kwa kiongozi mpya kuendeleza sera na mikakati iliyowekwa na uongozi uliokuwapo madarakani. Rais mpya ana uamuzi wa kupanga mipango na mikakati mipya endapo ataona kwamba iliyopo itamkwaza.
Kubadilika katiba kwa nchi za Afrika ni jambo la kawaida, kwani imeshatokea mara nyingi kwa baadhi ya nchi, rais wake kubadili katiba ilimradi tu abaki kuendelea madarakani.
Kwa mujibu wa Machiaveli, kiongozi ana haki na wajibu wa kuhakikisha kwamba anaendelea kulinda madaraka yake hata ukifika muda wa kustaafu anayo haki ya kuongeza muda, kwani kutafuta kiongozi mwingine ni kazi kubwa sana.
Pengine Machiaveli alikuwa akizungumzia ufalme zaidi kuliko uongozi ambao msingi wake ni mkuonyesha njia na endapo kiongozi akishindwa kuonyesha njia anapaswa awapishe wengine nao wajaribu kuonyesha njia.
Lakini kwa mantiki ya Machiaveli, ni lazima uongozi uwe endelevu. Endelevu aliyoiainisha ni ya kung’ang’ania madaraka, kwake yeye, uongozi ni mali ya mtu, pengine amepewa na Mungu hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kumnyang’anya aliyepewa na Mungu.
Ipo dhana nyingine ya uongozi endelevu kwa mantiki ya ‘maliberali’ na siyo ya ‘marialisti.’ Katika falsafa za kiliberali uongozi ni mali ya umma si mali ya mtu na ni lazima uwe endelevu, yaani viongozi waliopo madarakani wanapaswa kutengeneza mfumo wa kupasiana kijiti, yaani wewe ongoza kwa miaka nane mathalan, wakati ukiwa madarakani hakikisha kwamba anapatikana mtu mwingine wa kushika pale utakapoachia na pengine kuendeleza yale uliyoyapanga na kukusudia kuyafanya lakini ukashindwa pengine kutokana na muda, na hili linafanyika duniani kote.
Lakini lipo jingine linalotia mashaka katika uongozi wa Afrika; hivi karibuni Rais wa Rwanda, Paul Kagame alipitisha sheria ya kinga ya Rais atakayeondoka madarakani kutoshtakiwa kwa kosa lolote lile alilolitenda wakati akiwa Rais. Hii ni ngumu kwa sababu kinga hiyo yaweza kutumika vibaya, Rais aweza kuua, kuiba/kuhamisha na hata kuangamiza kwa kujiamini kwamba hakuna chochote kitakachomkuta. Mfumo huu ni wa Alfa na Omega, kwamba Rais ndiyo mwisho. Dhana hii inapingana na ile dhana ya kwamba hakuna aliye juu ya sheria. Kagame hivi sasa yuko juu ya sheria, yeye ndiye mwanzo na ndiye mwisho!
Binafsi naungana na wale wanaofikiri kwamba kuna haja ya kubadilisha mfumo wa uongozi wa Afrika, kwani uliopo hivi sasa ni ‘mkorogovyogo’!

Hawra Shamte ni Mhariri wa Siasa wa gazeti la Mwananchi.
hshamte@mwananchi.co.tz
0754 849694

1 Maoni ya Wasomaji:

Anonymous Celana Hernia anasema...

However want to statement on few common issues, The website taste is great, the articles is in point of fact excellent. Vimax Canada

12:10 PM  

Post a Comment

<< Rudi mwanzo

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

  • The Citizen
  • Mwananchi
  • Mwanaspoti
  • Business Times
  • Majira
  • Daily News
  • Nipashe
  • The Guardian
  • The Express
  • Kiongozi
  • Uhuru/Mzalendo
  • Arusha Times
  • BLOGI ZA KISWAHILI

  • Bangaiza
  • Mwandani
  • Pambazuko
  • Damija
  • Mtafiti
  • Martha
  • Gaphiz
  • Swahili time
  • Miruko
  • Dira yangu
  • Msangimdogo
  • Jeff Msangi
  • Kasri la mwanazuoni
  • Kurunzi
  • Baragumu
  • Mawazohuru
  • Fikra Thabiti
  • Mtandaoni
  • Motowaka
  • Mkwinda
  • Ngurumo
  • Nyembo
  • Bwaya
  • Omega
  • Tafakari za Maisha
  • Nuru akilini
  • Mtandawazi
  • Mhujumu
  • Vijimamboz
  • Wakati wa Ukombozi
  • Kijiwe Joto
  • Watoto Wetu
  • Jungu kuu
  • Kisima cha Weledi
  • Jarida la Ughaibuni
  • Bhalezee
  • Sauti ya Baragumu
  • Kona yangu
  • Furahia Maisha
  • Bakanja
  • Terrie Swai
  • Fatma Karama
  • Kazonta
  • Binti Afrika
  • Blogu ya Kilimo
  • Ukombozi
  • Mwafrika
  • Digital Africa
  • Blogu ya lugha mseto
  • BLOGI ZA WAAFRIKA

  • BLOGAFRICA
  • BLOGU ZA WAAFRIKA
  • DIGITAL AFRICA
  • MAMA JUNKYARD'S
  • MSHAIRI
  • KENYAN PUNDIT
  • MONGI DREAMS
  • ISARIA MWENDE
  • CUNNING LINGUISTICA
  • ETHIOPUNDIT
  • MOCHALICIOUS
  • UNGANISHA
  • DEMOKRASIA KENYA
  • CHANUKA
  • BANKELE
  • MAARIFA/AKIEY
  • AFROMUSING
  • NEHANDA DREAMS
  • BLACK LOOKS
  • YUMMY WAKAME
  • AFRICAN OIL POLITICS
  • NUBIAN SOUL
  • SANAA
  • VIRTUAL INSANITY
  • MENTAL ACROBATICS
  • KENYA UNLIMITED
  • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

    April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

    Imetengenezwa na

    Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

    na inawezeshwa na