" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Thursday, July 31, 2008

 Mfumo wa uongozi na demokrasia Afrika, ni mkorogovyogo!

Na Hawra Shamte

UKIANGALIA mlolongo wa matukio, visa na mikasa ya viongozi wa Bara la Afrika, moja kwa moja utabaini kuwa mengi wafanyayo ni yale yaliyoainishwa katika falsafa za Niccolo Machiaveli, mwanafalsafa wa karne ya 15 aliyezaliwa Roma Italia.
Katika masuala ya uongozi wa umma, Machiaveli aliweka mkazo kwa kiongozi kung’ang’ania kuendelea kubaki madarakani, alisisitiza kwamba ‘ufalme’ au uongozi ni lazima ulindwe kwa nguvu zote, hata ikibidi kutumia jeshi ama kuua.
Kama ni utashi wao, viongozi wengi hasa wa Bara la Afrika wangependa waendelee kukaa madarakani daima dawama, kwao wao ukishakamata madaraka ni sawa na pingu za maisha, hadi ufe uzikwe.
Mifano tunayo mingi, Wapo akina Yoweri Museveni, Robert Mugabe, Omar Al Bashir, Husni Mubarak na wengineo. Sidhani kwamba ni lazima wajitangaze kuwa ni maraisi wa maisha, bali vitendo vyao vinatosha kuthibitisha hayo. Je, demokrasia ya uchaguzi na kupishana madarakani inatumikaje Afrika?
Pengine demokrasia ya aina hiyo si demokrasia ya waafrika, uongozi wa jadi ungetosha kujenga misingi ya uongozi na demokrasia, kwani hivyo ndivyo inavyoonyesha kihalisia. Kila anayeshika madaraka ikiwa atalazimika kuondoka madarakani ataweka mazingira ambayo kama ataondoka basi nafasi yake ishikwe na angalau na mtoto wake, mifano ya hao tunayo mengi.
Tumeshuhudia katika nchi nyingi za Kiafrika viongozi wakiwa wanabadilisha katiba, za nchi ilimradi tu waendelee kubaki madarakani, hata kama wananchi wameshawachoka. Mara ngapi tunasikia kwamba Rais fulani anataka kufanya mabadiliko ya katiba ili kuongeza muda wa Rais kukaa madarakani.
Ziko katiba zinazoweka vipindi vya urais, kwa mfano Tanzania kipindi cha Rais kukaa madarakani ni miaka mitano mara mbili, hii ina maana ya kwamba baada ya miaka kumi hata kama rais huyo anapendwa vipi ni lazima akabidhi uongozi kwa mwingine.
Uamuzi wa aina hiyo una faida zake na hasara zake, faida ni kwamba unaepusha kujenga himaya ya kifalme na kidikteta. Hasara yake ni kwamba mara nyingine inashindikana kumaliza ajenda na miradi ambayo Rais amejiwekea kwani miaka 10 si mingi na sera nyingi ni za muda mrefu.
Yawezekana mtu akajenga hoja kwamba uongozi ni mchakato, hivyo wengine watakaokuja badala ya aliyeondoka watauendeleza mchakato huo. Hiyo ni kweli na ndivyo inavyopaswa iwe, lakini si lazima kwa kiongozi mpya kuendeleza sera na mikakati iliyowekwa na uongozi uliokuwapo madarakani. Rais mpya ana uamuzi wa kupanga mipango na mikakati mipya endapo ataona kwamba iliyopo itamkwaza.
Kubadilika katiba kwa nchi za Afrika ni jambo la kawaida, kwani imeshatokea mara nyingi kwa baadhi ya nchi, rais wake kubadili katiba ilimradi tu abaki kuendelea madarakani.
Kwa mujibu wa Machiaveli, kiongozi ana haki na wajibu wa kuhakikisha kwamba anaendelea kulinda madaraka yake hata ukifika muda wa kustaafu anayo haki ya kuongeza muda, kwani kutafuta kiongozi mwingine ni kazi kubwa sana.
Pengine Machiaveli alikuwa akizungumzia ufalme zaidi kuliko uongozi ambao msingi wake ni mkuonyesha njia na endapo kiongozi akishindwa kuonyesha njia anapaswa awapishe wengine nao wajaribu kuonyesha njia.
Lakini kwa mantiki ya Machiaveli, ni lazima uongozi uwe endelevu. Endelevu aliyoiainisha ni ya kung’ang’ania madaraka, kwake yeye, uongozi ni mali ya mtu, pengine amepewa na Mungu hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kumnyang’anya aliyepewa na Mungu.
Ipo dhana nyingine ya uongozi endelevu kwa mantiki ya ‘maliberali’ na siyo ya ‘marialisti.’ Katika falsafa za kiliberali uongozi ni mali ya umma si mali ya mtu na ni lazima uwe endelevu, yaani viongozi waliopo madarakani wanapaswa kutengeneza mfumo wa kupasiana kijiti, yaani wewe ongoza kwa miaka nane mathalan, wakati ukiwa madarakani hakikisha kwamba anapatikana mtu mwingine wa kushika pale utakapoachia na pengine kuendeleza yale uliyoyapanga na kukusudia kuyafanya lakini ukashindwa pengine kutokana na muda, na hili linafanyika duniani kote.
Lakini lipo jingine linalotia mashaka katika uongozi wa Afrika; hivi karibuni Rais wa Rwanda, Paul Kagame alipitisha sheria ya kinga ya Rais atakayeondoka madarakani kutoshtakiwa kwa kosa lolote lile alilolitenda wakati akiwa Rais. Hii ni ngumu kwa sababu kinga hiyo yaweza kutumika vibaya, Rais aweza kuua, kuiba/kuhamisha na hata kuangamiza kwa kujiamini kwamba hakuna chochote kitakachomkuta. Mfumo huu ni wa Alfa na Omega, kwamba Rais ndiyo mwisho. Dhana hii inapingana na ile dhana ya kwamba hakuna aliye juu ya sheria. Kagame hivi sasa yuko juu ya sheria, yeye ndiye mwanzo na ndiye mwisho!
Binafsi naungana na wale wanaofikiri kwamba kuna haja ya kubadilisha mfumo wa uongozi wa Afrika, kwani uliopo hivi sasa ni ‘mkorogovyogo’!

Hawra Shamte ni Mhariri wa Siasa wa gazeti la Mwananchi.
hshamte@mwananchi.co.tz
0754 849694

 Prof. Masha:Watanzania walijibu swali lisilo kuhusu Shirikisho

Na Hawra Shamte

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Profesa Fortunatus Lwanyantika Masha anasema kwamba kwa bahati mbaya au kwa kutokutambua, Kamati iliyoongozwa na Profesa Samuel Wangwe haikuweza kuwaelekeza Watanzania swali halisi walilopaswa kulijibu ambalo ni je, tuharakishe Shirikisho la Afrika Mashariki? Badala yake, wananchi wakajibu swali la je, mnataka Shirikisho?

Akizungumza katika mjadala wa wazi katika Chuo Kikuu cha St. Augustine, tawi la Dar es Salaam, Prof. Masha alisema kamati ya Wangwe iliibua maoni na hisia nyingi kuhusu kazi ya kamati yenyewe; uamuzi wa kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki; na wasiwasi wa kuunda Shirikisho la nchi zinazotofautiana kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama.

Profesa Masha anasema pengine mkanganyiko kuhusu Shirikisho unatokana na kuwapo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ili kulitambua Shrikisho la Afrika Mashariki ni muhimu kutofautisha baina ya Shirikisho na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Watu wengi hawaoni tofauti baina ya jumuiya hizo mbili, na ndiyo maana kushindwa kwa EAC kunaunganishwa moja kwa moja na Shirikisho kwamba nalo laweza kushindwa kama ilivyoshindwa Jumuiya. Wasichokifahamu wengi ni kwamba malengo na utashi wa kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki ni tofauti na yale yaliyokuwapo wakati wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977,” anasema Prof. Masha.

Prof. Masha anaendelea kueleza kuwa ingawa hivi sasa ipo Jumuiya ya Afrika Mashariki na ambayo kimfumo inaweza kuwa na Umoja wa Forodha, Soko Moja na Sarafu Moja bila ya kuwa na Shirikisho la kisiasa.

“Dhamira ya kuwa na Shirikisho ni kuunda Taifa Moja la watu wa Afrika Mashariki.”

Prof. Masha anasema katika utangulizi wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inaelezwa wazi kwamba: “Nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zimedhamiria kuimarisha mahusiano yao ya uchumi, kijamii, kiutamaduni, kisiasa, kiteknolojia na mengine, kwa maendeleo ya haraka kwa nchi zote, kwa kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki; pamoja na umoja wa forodha na soko moja, baadaye sarafu moja na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.”

Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulishawasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na likauridhia mwaka 2000. “Kwa maana nyingine ni kwamba; Bunge la Tanzania pamoja na Serikali ya Tanzania wameisharidhia kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki. Kinachobakia ni mchakato wa kulifikia Shirikisho,” anaeleza Prof. Masha.

Agosti 28, 2004, wakuu wa Nchi wanachama wa EAC (Summit) waliunda kamati ya kuangalia namna ya kuharakisha mchakato wa Shirikisho ili kutimiza kwa haraka kusudio la Shirikisho la Kisiasa. Ndipo ilipoanzishwa Kamati ya Amos Wako ambayo ripoti yake ilisema kwamba kimsingi kuundwa kwa Shirikisho la Kisiasa kumekwisha anza kwani tayari miundombinu yake imeshawekwa; kuna Mahakama ya Afrika Mashariki, Bunge la Afrika Mashariki pamoja na maelewano ya mahusiano katika mambo ya majeshi, usalama na sera za nchi za nje.

Ripoti ya Wako iliweza kuainisha majukumu sita ya Shirikisho ambayo ni Ulinzi na Usalama, mambo ya Nchi za Nje, Mamlaka ya Ziwa Viktoria, Haki, Polisi na Uhamiaji, fedha na Mipango na Miundombinu.

“Ingawa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawakuazimia moja kwa moja kukubaliana na mapendekezo ya kamati ya Wako, kwa matamshi yao walifurahishwa na kazi ya Kamati hiyo. Kwa kuwa mengi ya yaliyomo katika mikakati ya maendeleo (EAC Development Strategy 2006 – 2010) yanatokana na mapendekezo ya kamati ya Wako; kimsingi walikubaliana na programu ya kufikia Shirikisho kama ilivyopendekezwa na Kamati ya wako.”
Utata wa kazi ya kamati ya Wangwe
Kamati ya Wangwe ilihusika na mchakato wa Mashauriano ya Kitaifa (National Consultative Process) kuhusu kuharakisha Shirikisho la Kisiasa. Profesa Masha anasema nia ya kushirikisha wananchi wa Afrika Mashariki katika mchakato wa kuunda Shirikisho ni nzuri, ugumu ni namna ya kuwashirikisha na hasa baada ya maamuzi ya msingi yakiwa tayari yameisha chukuliwa. Ni taratibu zipi zitumike katika kuwashirikisha? Washirikishwe au waamue?

Prof. masha anasema pamoja na kuwa Kamati ya Wangwe ilikuwa inaratibu/inatafuta maoni ya wananchi kuhusu swali “je, Shiriksho liharakishwe au hapana?” lakini ilikuwa na utata wa aina mbili: Kwanza; mkanganyiko wa swali lililotakiwa kujibiwa. Pili; namna ya kupata maoni ambayo yanafanana na maoni ya Watanzania kwa ujumla. Yote mawili yalikuwa matatizo ya kiufundi.

Waliohudhuria mikutano ya Kamati ya Wangwe na wengi waliotoa maoni katika vyombo vya habari, walijibu swali tofauti, yaani: Je, tuingie katika Shirikisho au hapana? Kwanini?

“Tofauti hii kubwa kati ya swali lililoulizwa na swali lililojibiwa, ilileta mkanganyiko mkubwa, Waliokuwa wanaelewa vema Kazi ya kamati hiyo, waliliona zoezi lililoendeshwa na Kamati ya wangwe halikuwa na maana,”
Prof. Masha anasema.
Prof. Masha pia anabainisha tatizo jingine kubwa katika zoezi la Kamati ya Wangwe, kwamba lilikuwa namna walivyoratibu maoni ya wananchi. “Kwa mfano; walikwenda katika Wilaya yenye watu zaidi ya 300,000; wakapata ukumbi katika makao makuu ya Wilaya; wakafanya mkutano mmoja au miwili na kupata jumla ya watu 200. Maoni ya hawa 200 yana uhalali gani kuchukiliwa kwamba ni maoni ya wilaya nzima? Hawa 200 wamepatikanaje hata waweze kusemea Wilaya nzima? Anahoji Prof. Masha.

Hata hivyo, Prof. Masha anakiri kwamba jambo zuri lililotokana na mizunguko ya Kamati ya Wangwe ni kutoa mjadala katika taifa, uliosisimua kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki hata kama wanaanchi walijibu swali lisilo.

Mwisho Prof. Masha anatoa usahuri kuwa suala la Shirikisho ni suala la kisiasa, lenye kuhitaji maamuzi ya kisiasa. Wanasiasa hawawezi kukwepa wajibu wao wa kaumua mambo neyti kama Shirikisho, kwa kujificha nyuma ya kamati ambazo zina utata.

Mwisho.

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

  • The Citizen
  • Mwananchi
  • Mwanaspoti
  • Business Times
  • Majira
  • Daily News
  • Nipashe
  • The Guardian
  • The Express
  • Kiongozi
  • Uhuru/Mzalendo
  • Arusha Times
  • BLOGI ZA KISWAHILI

  • Bangaiza
  • Mwandani
  • Pambazuko
  • Damija
  • Mtafiti
  • Martha
  • Gaphiz
  • Swahili time
  • Miruko
  • Dira yangu
  • Msangimdogo
  • Jeff Msangi
  • Kasri la mwanazuoni
  • Kurunzi
  • Baragumu
  • Mawazohuru
  • Fikra Thabiti
  • Mtandaoni
  • Motowaka
  • Mkwinda
  • Ngurumo
  • Nyembo
  • Bwaya
  • Omega
  • Tafakari za Maisha
  • Nuru akilini
  • Mtandawazi
  • Mhujumu
  • Vijimamboz
  • Wakati wa Ukombozi
  • Kijiwe Joto
  • Watoto Wetu
  • Jungu kuu
  • Kisima cha Weledi
  • Jarida la Ughaibuni
  • Bhalezee
  • Sauti ya Baragumu
  • Kona yangu
  • Furahia Maisha
  • Bakanja
  • Terrie Swai
  • Fatma Karama
  • Kazonta
  • Binti Afrika
  • Blogu ya Kilimo
  • Ukombozi
  • Mwafrika
  • Digital Africa
  • Blogu ya lugha mseto
  • BLOGI ZA WAAFRIKA

  • BLOGAFRICA
  • BLOGU ZA WAAFRIKA
  • DIGITAL AFRICA
  • MAMA JUNKYARD'S
  • MSHAIRI
  • KENYAN PUNDIT
  • MONGI DREAMS
  • ISARIA MWENDE
  • CUNNING LINGUISTICA
  • ETHIOPUNDIT
  • MOCHALICIOUS
  • UNGANISHA
  • DEMOKRASIA KENYA
  • CHANUKA
  • BANKELE
  • MAARIFA/AKIEY
  • AFROMUSING
  • NEHANDA DREAMS
  • BLACK LOOKS
  • YUMMY WAKAME
  • AFRICAN OIL POLITICS
  • NUBIAN SOUL
  • SANAA
  • VIRTUAL INSANITY
  • MENTAL ACROBATICS
  • KENYA UNLIMITED
  • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

    April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

    Imetengenezwa na

    Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

    na inawezeshwa na